maombi na aina zake.
Maana ya Maombi:
Maana ya maombi ni kusema na Mungu au kuhitaji msaada toka kwa Mungu. Isaya 43:26, Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako.
Unikumbushe – Mungu anaposema tumkumbushe hana maana kuwa amesahau. Hapana. Ila anataka kuona moyoni umeweka nini. Ndiyo maana aliwaambia wana wa Israel kuwa “Niliwazungusha makusudi ili nione mioyoni mwenu mna nini.” Ndiyo maana tunatakiwa kuliweka Neno la Bwana mioyoni mwetu. Zab 119:10
Tuhojiane – Ni jambo la kumshukuru Mungu anayetupatia nafasi ya kueleza mambo yetu, kero zetu na shida zetu kwake kwa kuhojiana naye ili tupate kupewa haki zetu.
Haki zetu:
Katika Biblia ziko haki zetu nyingi sana ambazo Mungu wetu ametuahidi. Lakini bahati mbaya nyingi hatuzijuwi. Inatubidi kusoma Biblia kwa bidii ili Neno lake Kristo likae kwa wingi ndani yetu. Biblia ina mistari 31,173. Hebu jipime uone, wewe unaijua mingapi? Dan 9:1 – Daniel katika wakati wake alisoma kitabu alichokuwa ameandika nabii Yeremia akakuta muda ambao walitakiwa watoke utumwani umepita na bado wako utumwani. Walikuwa huko kwa kutokujua. Kwa hiyo kusoma Neno la Mungu kuna faida nyingi, muhimu ikiwa ni kufahamu ukweli wa mambo.
Sababu za Kuomba:
Ziko sababu mbali mbali za kusema na Mungu. Na kama tulivyoona hapo juu kuomba ni kusema na Mungu. Hii ina maana unapotaka kusema na Mungu ni vizuri ujuwe unataka kusema naye kuhusu nini. Tuchukue mfano: Unapoenda ofisi ya mtu ye yote, huwezi kuingia ofisini hapo wakati hujuwi unakwenda kwa sababu gani. Ndiyo maana ukiingia unaambia ‘karibu, tukusaidie nini?’. Ni kawaida kwamba jibu la swali hilo huwa lipo. Lakini watu wengi humwendea Mungu wakati hawajuwi sababu ya kumwendea. Pia, kwa kuwa Mungu ni baba yetu hatutakiwi kumwendea wakati wa shida tu, yaani shida ikiisha, basi. Hapana. Japo kwenye ofisi za watu huenda wakati tunashida tu, lakini kwa Mungu wetu tunatakiwa kwenda wakati wote. Hii huonyesha ushirika uliopo kati yetu na Yeye.
Sababu za kusema na Mungu, yaani sababu za maombi ni nyingi sana. Yako mambo mengi sana ambayo tunatakiwa kuyabeba wakati wa maombi. Ni vigumu kuyataja yote lakini tutaangalia baadhi, ambayo yatafanyika kama kielelezo. Lakini kwanza tuangalie maandiko, ndipo tutaendelea:
Kolosai 4:2-4 inasema hivi, Dumuni katika kuomba huku na shukurani, mkituombea na sisi pia, kwamba Mungu atufugulie mlango kwa lile neno lake, tunene siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake nimefungwa, ili niidhihirishe, kama inipasavyo kunena.
Hayo mambo mazito hapo juu ni maagizo ambayo Paulo aliwaandikia Wakolosai. Napenda tujifunze kutokana na hayo maombi. Mara nyingi watu wa Mungu husema tuko kwenye maombi, hata wakati mwingine tunakosea maana si jambo la kutangaza. Maandiko hayo yanatupatia mwelekeo wa sababu za kutupeleka mbele za Mungu kwa maombi. Pamoja na sababu hizo chache, hapo, pia tunaambiwa kuwa tunatakiwa kudumu katika kuomba, kudumu ni kutokata tamaa, kutokuchoka, kutokupunguza. Katika maneno hayo Mtume Paulo aliwaomba Wakolosai wawaombee pia. Unajua tunafanya makosa makubwa kama hatutaombea viongozi wetu. Tutawaombea nini? Mungu awafungulie milango, Mungu awape usemi, Mungu awawezeshe katika kunena na kutenda pia. Je, hayo ndiyo tutaombea kila siku? Hapana. Ni pamoja na hayo. Tutaona kwa kirefu baadhi ya mambo mengine ambayo tunapaswa kuyaombea, maana kama ni hayo tu basi nadhani ni muda mfupi tu nasi tutakuwa tumemaliza.
Tuangalie tena 1Yohana 5:14-15 Na huu ndio ujasiri tulionao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawa sawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.
Ujasiri wetu unaotupeleka kwenye maombi ndio huo. Mtu jasiri haogopi, hana mashaka hata kidogo. Kwa hiyo tunapaswa kuwa majasiri kwa Mungu wetu. Mahali pengine Biblia inasema mwenye haki ni jasiri kama simba. Uajua simba ni mnyama wa ajabu sana. Si mwoga. Hafanani na fisi. Ukiwa karibu na fisi ukamshtua kile anafanya ni kukuharishia: ishara ya uoga. Lakini ukimshtua simba, yeye hakimbii. Ni kama ndiyo unamwita kuwa aje mkutane.
Maandiko yanasema pia tuombe sawa sawa na mapenzi ya Mungu. Ni vizuri tufahamu mapenzi ya Mungu. Tutayapata wapi? Mapenzi ya Mungu tutayajuaje? Mapenzi ya Mungu yako kwenye Neno lake. Ebu tuangalie maandiko machache yanayohusu mapenzi ya Mungu. Na haya tunaweza kuyatumia kama muongozo wa maombi yetu wakati tunapoomba.
1Tim 2:1-4, Basi, kabla ya mambo yote, nataka dua, na sala, na maombezi, na shukurani zifanyike kwa ajili ya watu wote; kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu. Hili ni zuri, nalo lakubalika mbele za Mungu mwokozi wetu, ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli.
Hapo tunaona wajibu wetu. Tunatakiwa kuwaombea watawala wetu, wafalme wetu, ili tuishi kwa amani. Vinginevyo amani hutoweka. Amani inatakiwa kuendelea kuwepo kwa ajili ya maombi ya watakatifu. Pia anasema tuombee watu wote. Mpendwa ukweli Mungu anapenda watu wote, na anapenda wote waokolewe. Tunachotakiwa kuendelea kufanya ni kuwaombea. Anzia na wale unaowafahamu, ambao bado hawajaokoka. Waombee, ukijua kuwa na wewe kuna mtu alikuombea ukapata wokovu. Kumbuka pengine ulivyokuwa mbishi, hukutaka hata kusikia habari za wokovu. Pengine uliwafukuza waliokushuhudia habari za wokovu. Je, waweza kujua kwa nini uliokoka? Jibu: uliombewa na mtu.
Sasa zifuatazo ni baadhi ya sababu za maombi,
1. Isaya 62:7, Wala msimwache akae kiimya, mpaka atakapofanya imara Yerusalem, na kuufanya kuwa sifa duniani.
Maandiko yanasema tusimwache akae kimya. Ina maana tuendelee kuomba. Hivyo hayo ni mapenzi ya Mungu kwetu.
2. Zaburi 122:6, Utakieni Yerusalem amani, na wafanikiwe wakupendao.
Mpendwa, Baraka zingine ni za kuchukua tu, wala hazina gharama sana. Kutamka tu kwamba tunaitakia amani, tunaiombea amani Yerusalem, hizo ni Baraka za mafanikio; andiko linasema wafanikiwe wakupendao.
Kuna watu hawataki kusikia Israel. Wengine husema wataifuta katika ramani ya dunia hii! Huwa nacheka kwa kuwa kwa kusema hivyo huwa wanasema: Watamfuta Mungu kutoka katika uso wa dunia. Ukweli huwa hawajuwi wanasema nini. Mungu alimwambia Ibrahimu kuwa yeye atakaye kulaani nitamlaani, yeye atakayekubariki nitambariki. Ebu tujipatanishe na wateule wa Mungu kama tunataka kupona. Pia Mungu alisema ‘mpaka mtakapogundua dunia hii inakaa kwenye nini’, hapo ndipo atakapoiacha Israel wasiwe watu wake. Yeremia 31:35-37, Bwana anasema hivi, awapaye watu jua, ili kuwa nuru wakati wa mchana, na amri za mwezi na nyota, ili kuwa nuru wakati wa usiku, aichafuaye bahari, hata mawimbi yake yakavuma, Bwana wa majeshi, ndilo jina lake. Amri hizi zikiondoka, zisiwe mbele zangu, asema Bwana, ndipo wazao wa Israel nao wataacha kuwa Taifa mbele zangu milele. Bwana asema hivi, kama mbingu zikiweza kupimwa, na misingi ya dunia ikiweza kugunduliwa huko chini, ndipo wazao wa Israel pia nitawatupilia mbali, kwa ajili ya hayo yote waliyoyatenda, asema Bwana.
Mpendwa, mtu asikudanganye, ukasema vibaya juu ya Israel. Hii pia ni sawa na kusema vibaya juu ya mcha Mungu ye yote. Wala usithubutu kufungua kinywa kumnena mabaya. Nikukumbushe kidogo habari ya wale waliofungua vinywa kumnena vibaya Musa, walikuwa Miriamu na Haruni. Nakuambia Mungu aliingilia kati mwenyewe, akawaadhibu mara moja. Miriam akapigwa na ukoma. Kwa hiyo tujiepushe kulisema vibaya Taifa hilo la Mungu. Ni lake. Sikia Mungu anavyosema: ‘kama mtu atajua dunia imekaa juu ya nini ndipo Taifa hilo liaacha kuwa Taifa lake.’
3. Luka 6:28, Wabarikini wale ambao wawalaani ninyi, waombeeni wale ambao wawaonea ninyi.
Mpendwa, safari ya mbinguni imeelekezwa vizuri namna ya kuisafiri. Hiyo ni njia moja wapo ya kuelekea huko: Kuwaombea wale wanaowaonea, kuwabariki wale wanaowalaani! Fanya hivyo na Mungu atakubariki.
4. Luka 22:40, Alipofika mahali pale aliwaambia, ombeni kwamba msiingie majaribuni.
Bwana akawaambia kuwa waombe ili wasiingie majaribuni. Hakusema ‘ombeni kwamba msijaribiwe’. Aliwaambia waombe kuwa ‘wasiingie’. Maana yake nini? Unaweza kufika nyumbani kwa mtu, kwa nje, wala usiingie ndani. Waweza kufika Ubungo, ambapo tunajua ni Dar es salaam. Lakini ukifika Ubungo, bado utakuwa hukuingia mjini. Ebu tuombe kuwa tusiingie katika majaribu, mpaka yakatumeza na kutushinda.
5. 2Kor 13:7, Nasi twamwomba Mungu, msifanye lolote lililobaya, si kwamba sisi tuonekane tumekubaliwa, lakini ninyi mfanye lililojema, tujapokuwa sisi tu kama waliokataliwa.
Omba kuwa usifanye lolote lililobaya, yaani usifanye dhambi. Pia ombea watu uwajuao na usiowajua wasifanye dhambi. Hiyo itawasaidia wengine kujilinda na itafanya watu wengine wawe na breki katika kutenda maovu.
Omba watu wafanye yaliyo mema, ni pamoja na wewe mwenyewe, omba kuwa ufanye mema.
6. Filipi 1:9, Na hii ndio dua yangu, kwamba pendo lenu lizidi kuwa jingi sana, katika hekima na ufahamu wote.
Omba kuwa upendo wako uzidi kwa watu, omba kuwa upendo wa watu kwa wenzao uzidi kuwa mwingi sana. Unajua mpendwa Neno linasema siku za mwisho upendo wa wengi utapoa: utapoa wao kwa wao, utapoa kwa Mungu. Sasa omba kuwa watu wapendane. Omba kuwa watu wampende Mungu wao aliye waumba. Wasimpende adui ambaye hakuwaumba.
7. 1Thes 5:23, Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.
Ndugu mpendwa, haya ni maombi ya muhimu sana. Kama Biblia isemavyo kuwa Yesu atakuja kama mwivi. Ni wazi kabisa tunafahamu kuwa mwizi hatoi taarifa ya kuwa anakuja kuiba, labda jambazi. Jambazi anaweza kutoa taarifa maana huwa anakuja akiwa tayari kwa lolote lile. Bwana alisema atakuja kama mwivi. Kwa hiyo tunatakiwa kuomba kuwa wakati wa kuja kwake, tusiwe na kasoro katika miili yetu, nafsi zetu na roho zetu.
8. Luka 11:13, Basi, ikiwa ninyi mlio waovu mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vilivyo vyema, je! Baba aliye mbinguni hatazidi sana kuwapa Roho mtakatifu hao wamwombao?
Wapo watu wengi ambao hukaa muda mrefu kabla hawajajazwa na Roho Mtakatifu, mpaka wengine wanakata tama na kudhani Roho mtakatifu ni wa watu maalumu. Hapa. Wala usikate tamaa, endelea kuomba huku ukiamini kuwa Mugu atakupatia Roho mtakatifu. Pia inawezekana unanena kwa lugha, ambayo wengi wamedhani kila anayenena kwa lugha ana Roho wa Mungu. Mpendwa, ebu kagua kama kweli ni Roho wa Mungu. Maana hata waganga wa kienyeji wananena kwa lugha. Tofauti iliyopo ni kwamba hawana matunda ya Roho mtakatifu. Usiridhike na lugha tu isiyo na matunda, maana imeandikwa: Mtawatambua kwa matunda yao. Math 7:16
9. 1Kor 14:13, Kwa sababu hiyo yeye anenaye kwa lugha na aombe apewe kufasiri.
Ziko haki zetu nyingi katika Biblia ambazo hatujazifahamu. Na kama hatuzifahamu, basi, hatuwezi kuziomba. Lakini hapa tunaambiwa kuwa mtu anayenena kwa lugha aombe pia apewe kufasiri. Fanya hivyo na Mungu atakujalia kufasiri.
10. Zab 37:4, Nawe utajifurahisha kwa BWANA, Naye atakupa haja za moyo wako.
Wakati mwingine huwa tunayo yale tunayoyawaza mioyoni mwetu, bila mtu mwingine kujua. Tunapaswa kumuomba Bwana atupatie haja ya mioyo yetu. Ni kweli kuwa Mungu anajua yote. Lakini anapenda kusikia tukimwambia. Yesu akamuuliza Baltmayo kipofu kwamba “wataka nikufanyie nini?” Akasema nipewe kuona, akapewa kuona. Marko 10:51
11. Zab 71:9, Usinitupe wakati wa uzee, Nguvu zangu zipungukapo usiniache.
Mpendwa, hili ni ombi muhimu sana katika maisha yetu. Unajua wako watu wanaishi kama Wafalme wa zamani. Wafalme wa zamani waliishije? Walikuwa wanasalimiwa ati ‘Uishi milele ee mfalme’. Hawakuwa wanajiandaa kuwa kwa vyovyote wataondoka katika utawala. Hawakujua kabisa kuwa siku moja nguvu zao zitakwisha.
Natumaini unakumbuka jinsi Herode alipopata taarifa kuwa mfalme mwingine amezaliwa, yeye alipanga namna ya kumwangamiza. Mfalme aliyezaliwa akiwa kitoto kichanga ingemchukua miaka mingi kufikia umri wa kutawala kama mfalme. Na inawezekana kabisa hadi afikie umri huo wa kutawala, yeye Herode tayari angekuwa ameshakufa. Lakini kwa sababu ya kufikiri ataishi milele kweli, kama ambavyo alikuwa akisalimiwa, yeye akaona cha kufanya ni kumuangamiza mfalme-mtoto huyo kwa kuwa yeye Herode ataendelea kutawala milele. Ni ajabu kabisa!
Hebu tuone maombi hayo ya Daudi katika Zaburi 17:9 yalivyokuja kufanya kazi. Tunapata habari hiyo katika 2Sam 21: 15-17, Basi kulikuwa na vita tena kati ya Wafilisti na Israel; Daudi akashuka mpaka Gobu, na watumishi wake pamoja naye, akapigana na Wafilisti, naye Daudi akaishiwa na nguvu. Naye Ishi-benobu, aliyekuwa mmojawapo wa Warefai, ambaye uzito wa mkuki wake ulikuwa shekeli mia tatu za shaba kwa uzani, naye amejifungia upanga mpya, alijaribu kumwua Daudi. Lakini Abishai, mwana wa Seruya, akamsaidia, akampiga Mfilisti akamwua. Ndipo watu wa Daudi wakamwapia, wakasema, Wewe hutatoka tena pamoja nasi kwenda vitani, usije ukaizima taa ya Israel.
Maombi aliyoyaomba Daudi mtumishi wa Mungu kuwa atakapokuwa mzee, yaani nguvu zake zitakapokwisha asiachwe, siku ilifika kweli nguvu zake zikaisha. Akakaa chini. Ndugu yangu, mwanaume Daudi alishindwa hata kukimbia, achilia mbali kupingana. Huyu ni Daudi aliyeua dubu, aliyeua simba, Daudi aliyeua Goliathi!
Ndugu yangu siku zinakuja, wengine tayari zimewafikia, hawawezi tena kuomba kama walivyofanya zamani. Hawawezi tena kuhubiri kama walivyofanya zamani. Nguvu zao zimekwisha. Hata wanapokabiliana na Ishi-benobu wao, hawawezi tena.
Japo Ish-benobu alikuwa ana upanga mpya, maana yake mbinu mpya tofauti na ile aliyoizoea enzi zake, lakini kifo kilikuwa kinamkabili. Daudi aliwahi kuomba zamani na sasa faili lake likafunguliwa, likakutwa kuna ombi hilo ambalo halikuwa limejibiwa hadi wakati huo. Na ndipo ilibidi jibu litumwe. Ndugu yangu, nikipiga picha jinsi Daudi alivyokuwa amekaa chini, anamwangalia Ishi-benobu mbele yake, bila shaka alikuwa anamwambia ‘siku zako zimekwisha…..Wewe ni halali yangu’. Kumbuka vijana wote walikuwa wamekimbia hivyo Daudi alikuwa amebaki peke yake.
Yawezekana hapo ulipo uko peke yako, huna mtu wa kulia kwako wala kushoto kwako. Ni vita mbaya sana hiyo. Huna hata mtu wa kumwambia jambo, kuwa nikifa watazame kitu muhimu nimekiweka mahali. Kumbuka wakati huo Daudi alikuwa na ramani ya Hekalu, wala asingeweza kumpatia Ishi-benobu maana haikuwa inamhusu.
Pengine sasa Ishi-benobu yuko mbele yako, unachokiona ni upanga mpya! Sikia Neno toka kwa Bwana Mungu wako, hatayaabisha mafuta aliyokupaka, kamwe. Pamoja na maombi yako kuwa asikuache, lakini nasema Mungu alikupaka mafuta, WEWE ULIYE KATIKA NJIA HII YA WOKOVU, hatakuaibisha. Hataaibisha mafuta aliyokupaka. Abishai hayuko mbali. Kaza macho yako juu, kuna jambo litatokea. Kabla Ishi-benobu hajakufikia, Abishai atakutokea. Bwana ameshasema na Abishai. Namuona katika ulimwengu wa roho anakuja mbio. Ole wa Ishi-benobu, mauti imemkaribia sana. Usiogope. Abishai huyo, anakuja. Hutaaibika. Vita ni vya Bwana! 2Nyakati 20:15
Aina za Maombi:
Maombi yamegawanyika katika aina kadhaa. Tutaziangalia hapa chini kama ifuatavyo.
1.Maombi ya Vita
Tunajua kabisa tuko vitani katika maisha yetu. Na peke yetu hatuwezi kupigana vita hii. Kwa hiyo ni lazima tumshirikishe Mungu vita hii. 1Tim 6:12 – Piga vita, 2Kor10:4- Silaha za vita vyetu.
Tunapokuwa kwenye maombi haya ya vita, tunatakiwa kuelewa mambo yafuatayo:
a). Tuwajue vizuri maadui zetu tunaopigana nao.
b). Tuzijue silaha ambazo Mungu ametupatia.
c). Tujifunze vizuri namna ya kutumia silaha zetu, vinginevyo silaha hizo zitageuka kutudhuru sisi. (Ukitupa bomu la mkono vibaya litakulipukia wewe mwenyewe).
d). Tuzijue vizuri silaha anazotumia adui yetu.
Maombi haya ya vita ni maombi ya wakati wote wa uhai wa binadamu, kwa kuwa vita hii katika ulimwengu wa roho hukoma pale tu mtu anapokufa.
2. Maombi ya Toba
Maombi haya ya toba yanatakiwa yafanywe kwa makini sana. Yohana 9:31 inasema Mungu hawasikii wenye dhambi. Maombi ya toba ni maombi ya kujutia yale tuliyoyafanya ambayo hayakumpendeza Mungu. Lengo la maombi haya ni kuungama makosa tunayoyajua na tusiyoyajua na kuamua kutokuyarudia tena na kuomba Mugu atuepushe kufanya makosa tusiyoyajua.
Yohana 8:11, …Usitende dhambi tena!. Pia Yohana 5:14. Katika maandiko haya kuna kielelezo cha toba. Mwanamke alikamwatwa kwenye zinaa na akaletwa kwa Yesu akishitakiwa. Walitaka kumpiga kwa mawe lakini Yesu alimsaidia. Neno linasema Yesu aliinama akawa anaandika chini, japo haikuelezwa alikuwa anaandika nini. Lakini wanatheolojia wanasema, yawezekana alikuwa anaziorodhesha dhambi za kila mmoja aliyekuwa pale, hao ambao walitaka kumpiga kwa mawe yule mwanamke. Wote walipojiona wakakimbia. Na yule mwanamke akabaki peke yake na Yesu. Na ndipo alipoambiwa maneno hayo: Usitende dhambi tena!
Tunamwona pia mtu aliyekuwa amelala kwa mika 38, katika birika la Bethzatha [Yohana 5:2-9]. Kulala kwa miaka 38 inaonyesha mtu huyo anayo sifa ya uvumilivu, ambayo wengi wetu tunashindwa. Tunaamua kuhama hama kutafuta hiki na kile. Yesu alimkuta yule mtu akiwa amelala na akamuuliza, Unataka kuwa mzima? Nadhani jibu lake lilikuwa jepesi, tena rahisi: Ndiyo! Lakini ona anavyozunguka: ‘Mimi sina mtu wa kunitia birikani, ninapotaka kuingia mwingine hunitangulia’ Alikuwa hajaulizwa kama ana mtu wa kumtia birikani wala hakuulizwa kwa nini haingii kwenye birika, hakuulizwa kwa nini haponi. Hayo maswali ndiyo yangejibiwa kama alivyojibu. Lakini yeye aliulizwa, ‘Unataka kuwa mzima?’
Hili ni tatizo la watu wengi wanapokwenda kwenye maombi. Badala ya kufanya toba ya kweli, wanabaki kuzunguka. Mwanzo 3:11-12, Ni nani aliyekwambia kuwa uko uchi? (Nimejiona); Je, umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? (Ndiyo). Lakini hapa Adamu alijibu, ‘Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda nikala’.
Swali, kwenye Mwanzo 3:13, Bwana Mungu akamwambia mwanamke, Ni nini hili ulilofanya?. ( angejibu Nimekula tunda au nimempelekea Adamu au nimemkosesha Adamu). Lakini yeye Hawa alijibu ‘Nyoka amenidanganya nikala’. Unaona hapa?
Mungu hakumuuliza nyoka swali bali alimpa adhabu tu. Kwa nini hakumuuliza? Mungu hakumuuliza nyoka kwa sababu Nyoka alikuwa amefanya kazi yake. Yeye huitwa Mjaribu, Mwongo, Mtega mitego nk. Hiyo ndiyo kazi ambayo shetani anafanya na amemwacha aendelee kufanya hivyo. Ndiyo maana Yesu akasema tuangalie mtu asitudangaye. Mathayo 24:4.
Katika maombi ya toba ni vema kuangalia sana tunavyoungama mbele za Mungu. Kuna uwezekano mkubwa tusitake kutubu makosa yetu bali tukaanza kutafuta yule aliyetukosesha. Toba sahihi ni ile ambayo mtu hujutia makosa yake yeye mwenyewe na kujiona ni yeye ndiye anahusika kwa makosa hayo. Hali hii ndiyo huleta toba yenye maana.
3. Maombi ya Kujilinda.
Efeso 6:13- Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana…... Wakati tunaposema ‘silaha’ inaonekana kama ni silaha za kushambulia. Lakini hebu nikuonyeshe kitu hapa:
Mungu anasema ‘vaeni silaha zote’: Kweli viunoni, Dirii ya haki kifuani, Utayari kwenye miguu, Ngao ya Imani, Chapeo ya wokovu, Upanga wa Roho (Neno) na Sala zote na Maombi. Silaha zilizotajwa hapo ni za kujilinda isipokuwa mbili tu ndizo za kushambulia adui, ambazo ni Upanga wa Roho na Sala zote na Mombi. Ndiyo maana nikasema ziko silaha za kujilinda:-
Kweli viunoni – Tunapaswa kuwa wakweli hata kama inatugharimu maisha yetu. Ndiyo maana Yohana 8:32 inasema hivi, Mtaifahamu kweli, nayo kweli itawaweka huru. Kuwekwa huru maana yake ni kutokuogopa chochote. Wakati mwingine tumeogopa wanadamu tukaanguka kwenye mtego. Mithali 29:25, Kuwaogopa wanadamu kunaleta mtego. Kwa kule kusema, kweli viunoni ana maana kweli ifungwe kiunoni kama unavyofungwa mkanda, isitoke. Ni baada ya kufungwa kweli viunoni ndipo tukakuwa wajasiri kama simba. Mithali 28:1, Waovu hukimbia wasipofuatiwa na mtu; Bali wenye haki ni wajasiri kama simba.
Dirii ya Haki Kifuani – Hili linajieleza lenyewe.
Utayari miguuni – Kwa sababu miguu ndiyo inayotembea. Hapa imetumiwa kuwakilisha utendaji. Ni wangapi mpaka sasa hawajafikiwa na Injili? Nani atawafikia? Ni yule aliye tayari kwa kutoa Muda wake, Fedha zake na hata maisha yake.
Ngao ya Imani – Siku zote adui yetu hutupa mishale, tena ya moto. Imani peke yake ndiyo itatusaidia tusidhurike na mishale hiyo anayoitupa. Imani ni muhimu sana na inawindwa ili tunyang’anywe.
Wakati wa misukosuko baharini kwenye mtumbwi Yesu aliwauliza wanafunzi wake, ‘Imani yenu iko wapi’?. Luka 18:18, Atakapokuja mwana wa Adamu ataikuta Imani? Yakobo 2:14-17, Imani bila matendo imekufa. Watu wengi wanaodai kuwa wanayo Imani, lakini matendo ya ile Imani hayaonekani, maana yake ni kwamba Imani hiyo imekufa.
Chapeo ya Wokovu – Chapeo ni kofia ngumu. Mwendesha piki piki hutakiwa kuvaa chapeo [Helmet] ambayo inaweza kumsaidia wakati wowote akianguka ili asiumie kichwa. Kichwani kuna vitu vingi, ikiwa ni pamoja na Ubongo. Ubongo ndio kiungo cha muhimu sana katika mwili wa binadamu. Ni sawa na kompyuta. Kumbukumbu zote ziko hapo kwenye ubongo. Hivyo panatakiwa kulindwa ili pawe salama. Na hapo ndipo palipo na uwanja wa vita kwa kuwa kabla mtu hajatenda dhambi yoyote: huona au husikia, hunusa au huonja kisha ubongo unatafakari. Na baada ya kutafakari nafsi ya mtu ikiruhusu lile lililotafakariwa likateremka moyoni, hapo ndipo moyo hufanya uamuzi wa ama kukataa au kukubali lile lililotafakariwa kisha mhusika huchukua hatua.
Sasa basi tumeona silaha hizo za kujikinga, tumalizie na silaha za Kushambulia.
Upanga wa Roho (Neno) – Naziita silaha za kushambulia kwa sababu ndizo tunatumia kumshambulia adui yetu. Tunampinga kwa neno. Yakobo 4:7, Basi mtiini Mungu, mpingeni shetani naye atawakimbia. Wako watu wengi ambao hujaribu kumpinga shetani kabla hawajamtii Mungu. Hiyo ni hatari. Kumbuka wana wa Skewa walijaribu kulitaja jina la Yesu mapepo yakawararuwa. Mdo 19:14 Kuna wakati tunapaswa kumshambulia adui akiwa mbali, kama vile kwa kutumia silaha aina ya mzinga. Hatutakiwi kumngoja hadi atuvamie ndipo tumpige.
Sala zote na Maombi – Hizo pia ni silaha za kushambulia. Maana tunatakiwa kuomba sawa na Neno la Mungu linavyosema. 1Yohana 5:14-15, Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake ya kuwa tukiomba kitu sawa sawa na mapenzi yake atusikia vema. Na kama tukijua kwamba atusikia tuombacho chote, twajua ya kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.
Tukiomba twapasa kuamini, kwa maana imeandikwa tukisitasita Mungu hawi na furaha na sisi. Pia katika Ebrania 11:6, Lakini pasipo Imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.
4. Maombi ya mahitaji ya kiroho na kimwili
Katika maisha yetu ya kila siku tunakutana na uhitaji wa vitu mbali mbali: Chakula, mavazi, malazi, uponyaji nk. Neno la Mungu linatuelekeza pia kuomba juu ya mambo kama haya. Luka 6:9-15. Natumaini hili halihitaji maelezo mengi kwa kuwa linajitosheleza.
Baada ya kuwa tumeona aina mbali mbali za maombi sasa tuangalie Makundi makuu Mawili ya maombi.
Maombi, katika ujumla wake, yamegawanyika katika makundi mawili ambayo ni MAOMBI YASIYO NA UKOMO na MAOMBI YENYE UKOMO. Kwa maneno mengine ni maombi ya kudumu na maombi yasiyo ya kudumu.
Maombi yasiyo na Ukomo:
Katika 1Thes 5:17 tunapata maneno haya: Ombeni bila kukoma. Andiko hili ni kwa ajili ya maombi ambayo hayana mwisho. Mwisho wa maombi haya ni pale tutakapofika nyumbani kwa Baba yetu. Katika Luka 18:1 imeandikwa, Akawaambia mfano ya kwamba imewapasa kumuomba Mungu siku zote wala wakikate tamaa. Neno linasema tuombe bila kukoma. Neno linasema pia tuombe Mungu siku zote wala tusikate tamaa.
Kama nilivyosema mahali fulani kuwa tunapigana vita, na kamwe shetani hataacha vita mpaka atakapotupwa motoni. Hii ina maana siku zote tutaendelea kuwa na vita, na kama ndivyo hivyo lazima Tudumu katika Maombi. Maombi ya kudumu ni jumla ya maombi yote yanayohusu mambo ya rohoni: Toba, Vita, Kujilinda kwa kuwa tungali duniani, twakaa na watu mbali mbali huku safari ya mbinguni ikiwa inaendelea. Pia maombi kama vile kuombea amani ya miili yetu na nchi zetu ni maombi ya kudumu.
1Yohana 3:3- Kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa. Kujitakasa ni kitu endelevu. Mara nyingi twamkosea Mungu wetu kwa mawazo, maneno na matendo. Ndiyo maana baada ya kumjua Mungu vizuri Daudi alisema katika Zab 19:14 kwamba Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, yapate kibali mbele zako, Ee BWANA, Mwamba wangu na mwokozi wangu. Tunatakiwa kuyatafakari wakati wote maneno haya aliyoyasema Daudi mtumishi wa Mungu.
Maombi yenye Ukomo:
Katika Mathayo 21:22 tunapata maneno haya, Na yo yote mtakayoomba katika sala mkiamini, mtapoke. Mtu anayeomba kitu halafu akakipokea ni wazi kwamba hawezi kuendelea kukiomba tena. Mifano: mtu anayeomba Mungu ili apate mke/mume, baada ya kuwa ameoa/ameolewa hawezi kuendelea kuombea tena hitaji hilo. Mtu anapoomba kwa ajili ya kupata uponyaji, akiponywa hawezi kuendelea kuomba maana ameshapokea alichokuwa anahitaji. Kwa ujumla ni kwamba mtu anapokuwa anaombea hitaji fulani akilipokea huo ndio unakuwa mwisho wa ombi hilo.
Sasa, kwa kuangalia haraka haraka, ni rashisi mtu kusema kwamba Biblia inajipinga, kwa sababu kule inasema tuombe bila kukoma, halafu huku inasema tukiamini tutakuwa tumepokea. Na kama mtu akipokea kinachofuata ni kushukuru! Sasa kama tunatakiwa kushukuru kwa nini tena tuendelee kuomba bila kukoma? Jibu la wasi wasi huu ni hilo kwamba kuna mambo ambayo tunapoomba majibu yake ni dhahiri, na uhitaji huo huishia hapo. Lakini hata kama si dhahiri, yaani bado ni kwa Imani, lakini baada ya muda kitu hicho hudhihirika na hivyo kutokuwepo haja tena ya kuendelea kuombea kitu hicho hicho tena. Maombi yote yanayohusu mambo ya kimwili yako kwenye kundi hili. Kuna wakati tunatakiwa kuacha kuombea jambo fulani la kimwili hata kama hatukupata jibu lake. Maombi pia kama vile uhitaji wa kujazwa na Roho mtakatifu, kufanikiwa katika huduma fulani, nk, nayo yanaingia katika kundi hili.
Jambo jingine la kuzingatia katika maombi yenye ukomo ni kwamba siyo lazima jibu la maombi hayo liwe ni ndio. Kuna uwezekano wa mtu kuomba kitu ili apatiwe lakini Mungu akamwambia hapana! Na hapo ndiyo ukawa mwisho wa maombi ya kitu hicho. Tatizo kubwa ambalo hutokea sehemu hii ni kwamba kuna wakati mwingine watu huomba huku jibu wanalo tayari. Sasa inapokuwa imetokea kinyume na jinsi walivyoomba, ni rahisi sana wao kufikiri kwamba Mungu hajajibu, kwa kuwa walitaka Mungu ajibu kwa njia ambayo wao wanaona inafaa. Lakini kwa kawaida jibu la maombi yoyote linaweza kuwa Ndiyo, Hapana au Subiri. Na lolote katika hilo huwa ndilo ambalo Mungu Baba ameona kuwa linafaa.
Hebu tuangalie mfano mmoja katika 2Kor 12:7-10, Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo, nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi. Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke. Naye akaniambia Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu. Napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.
Ujumbe huo unajieleza wenyewe. Mtume Paulo aliomba mwiba mtoke. Hilo ndilo lilikuwa ombi lake na aliomba huku akitegemea jibu la ndio, kwa maana alikuwa anateseka. Ndiyo maana aliomba mara tatu: Mara ya kwanza hakuna jibu, akaomba tena mara ya pili, hakuna jibu, akaomba tena mara ya tatu ndipo Mungu akamwambia ‘hapana, kwa kuwa Neema yangu yakutosha’. Na baada ya jibu hilo yeye alifurahia kwa kuwa ndivyo Bwana alivyoona inafaa. Na ndipo baadaye akaja kuelewa sababu ya kutokuondolewa kwa mwiba huo: ili asije akajisifia kwa vile Mungu alivyokuwa akimtumia. Hali hiyo akaifurahia na akakubali matokeo! Na akawa tayari kukubali kubaki na mwiba huo hadi mwisho wa maisha yake. Lakini baada ya kujibiwa vile hakuendelea tena kumuomba Bwana aundoe mwiba huo. Maombi hayo yalifikia ukomo siku ile alipojibiwa.
Mfano mwingine unaofanana na huo unapatika katika kitabu cha Kumb 3:23-28 ambapo Musa mtumishi wa Mungu alimuomba Mungu ili aingie nchi ya Ahadi, [Kaanani] lakini Bwana Mungu alimkatalia.
Kutokana na mifano hiyo miwili tunajifunza kwamba tunapoomba jambo lolote kwa Mungu tunakiwa kukubali matokeo, huku tukijua kwamba kwa kuwa Mungu ni Baba yetu kamwe hawezi kutupatia nyoka badala ya samaki au jiwe badala ya mkate. Wakati wa kujibiwa ‘hapana’ inawezekana isiwe rahisi kuelewa lakini kwa kuwa tunayemwomba ni Baba yetu ni lazima atatufahamisha kwa nini ameleta jibu la ‘hapana’. Kwa kuwa ikiwa ni ndiyo au hapana, kama ni Mungu ndiye aliyejibu basi lolote kati ya hayo lengo lake ni jema kwetu!
Hayo ndiyo makundi makuu mawili ya maombi. Lakini katika maombi ya kundi lolote ni lazima kushukuru. Kwa yale yasiyo na ukomo ni lazima kushukuru kwa kuwa kila tunapokuwa tumeomba, kwenye hatua fulani, Mungu huwa ameshatenda. Lakini pia twapasa kumshukuru Mungu hata kwa yale ambayo atatenda. Kwa maombi yale yenye ukomo, tukipokea tulichokiomba ni vema tukamshukuru Mungu. Lakini hata kama tumekipokea kwa Imani tu na hakijadhirika kimwili, pia tunatakiwa kushukuru tu. Na shukurani hizi zinatakiwa kuendelea kuwepo hata kwa yale ambayo majibu yake ni ‘hapana’. Hivi ndivyo Biblia inavyosema katika 1Thes 5:18 kwamba Shukuruni kwa kila jambo, maana hayo ndiyo mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.
Dalili moja wapo ya siku za mwisho ni watu kukosa shukurani. 2Tim 3:2. Hebu tupende mkumshukuru Mungu kwa yale anayotutendea na yale atakayotutendea pia. Katika Luka 17:11-19 tunapata habari ya Bwana Yesu alipowaponya wale wakoma kumi (10) lakini ni mmoja tu ndiye aliyerudi kushukuru, mpaka Yesu mwenyewe akashangaa. Yule aliyerudi kushukuru aliambiwa na Yesu kwamba Imani yake Imemuokoa. Yaani tayari alishashugulikiwa na rohoni pia. Shukurani kwa Mungu ni jambo la mumihu sana kila tunapokuwa tumepeleka maombi mbele za Mungu
Shetani, ambaye ni adui yetu, anajua maandiko. Ndiyo maana alipomwendea Yesu ili amjaribu alitumia maandiko, akisema ‘imeandikwa..’. Katika siku za mwisho shetani atawafanya watu wasimrudishie Mungu shukurani, wakose kushukuru ama kwa kuwasahaulisha au kwa kuwafumba wasione chochote chema kutoka kwa Mungu. Mtu asiye na shukurani ni rahisi sana kuingiliwa na tabia ya kunung’unika, na manung’uniko si jambo jema mbele za Mungu.
Kwa hiyo katika yote tunayoomba ni lazima tuwe watu wenye kushukuru ili tusiingie katika kundi la watu wenye kutimiza maandiko.
Kama kuna swali lo unakaribishwa na kwa neema ya Mungu tutapata jibu lake.
Mungu akubariki.
By
Mr Aman Chombe

Comments
Post a Comment